Friday, September 20, 2013

GLOBAL PUBLISHERS WAMCHANA TENA UWOYA..SOMA HAPA


Na Luqman Maloto

BINAFSI nafahamu kwamba Irene Uwoya aliwahi kuwa staa mkubwa nchini lakini akafanya makosa na sasa ameshuka chati. Ameporomoka kwa kiasi kikubwa sana.

 Elizabeth Michael ‘Lulu’, baada ya ‘ajali’ yake na marehemu Steven Kanumba, alikaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini baada ya kutoka ameonekana kuwa na mafanikio makubwa kuliko Uwoya ambaye siku zote yupo mtaani.
Pengine kuna aina fulani ya maisha ambayo Uwoya amejichagulia maana akina Rose Ndauka, Aunt Ezekiel, Wema Sepetu na wengineo wamekuwa wakifanya vizuri, wanamfunika sana. Ameshindwa kujisahihisha, ataendelea kusugua.
Najua kwamba Uwoya ana hali mbaya kisanii, amechoka, muonekano wake hausisimui tena, amepoteza mashabiki, kwa maana hiyo hauzi. Dili za kucheza filamu zinaota mbawa kila kukicha, maprodyuza wanataka wakali ambao wanafanya biashara sokoni.
Naelewa kuwa hivi sasa katika ulimwengu wa masupastaa, Uwoya amebaki msindikizaji lakini sikuwahi kufikiri kwamba anaweza kufikia hatua mbaya kiasi hicho. Kafikishwa mbaroni kwa wizi wa simu? Yaani wizi wa simu ya mkononi! Anatia huruma.
Yamemfika yapi? Sitaki kuamini kama Uwoya anashindwa kununua simu halali. Akili nyingine inaniambia kuwa hawa dada zetu wanaharibiwa na uchu wa kupenda vitu vya juu lakini uwezo ni mdogo. Je, huo wizi wenyewe alifanyaje?
Atakapofikishwa mahakamani pengine itajulikana kama kweli amehusika na wizi huo, basi itafahamika ameufanyaje. Ni yeye moja kwa moja au kupitia kwa mtu mwingine? Dunia ina mengi, ni vizuri hili jambo likafika kortini, huko tutajua ukweli halisi.
Swali langu ni hili, kama kweli ile simu alinunua kwa nini pale kituoni hakutoa risiti? Hata kama ingekuwa nyumbani, alishindwa nini kuagiza aletewe kuthibitisha kama ni mali yake? Maswali hayo mawili yanaongeza uzani kwenye madai kwamba ile simu ni ya wizi.
Ni ya wizi sawa, je, ni kweli Uwoya anaweza kuiba simu? Inawezekana kabisa akatega Kariakoo halafu amvizie mtu na kumchomolea? Maana mashtaka dhidi yake ni Wizi wa Maungoni, yaani wizi wa kumchomolea mtu kitu kutoka mwilini.
Kesi ipo Msimbazi Polisi na imeandikwa kwenye kitabu cha ripoti za kumbukumbu (report book ‘RB’) kwa nambari MS/RB/8522/2013. Hata hivyo, simu yenyewe iliyoibwa ina thamani kubwa, nahisi Uwoya aliinunua kwa mtu ambaye ndiye mwizi.
Mikono ya Uwoya na vidole vyake vilivyo, haoneshi kama anaweza kuwa mkali wa kuchomolea watu. Hata kama kaishiwa na kupigika, siyo rahisi akafanya hivyo. Sura yake haioneshi ushujaa wa ‘kupiga ndole’ lakini ya Mungu mengi.
Labda kauziwa lakini yeye ndiye kakutwa na mali ya wizi (aliyekutwa na ngozi ndiye aliyeiba ng’ombe). Kama ipo hivyo, hilo nalo ni tatizo kubwa. Maana yake yeye naye ni mmoja wa watu wanaowafanya wezi waendelee kufanya uporaji. Anawafadhili kwa mlango wa nyuma.
Tusimamie hapa kwamba kama alinunua, basi Uwoya ni mfadhili wa wezi kwa sababu mtu anayenunua mali ya wizi, anawasaidia wezi kuendelea kuishi kwa uporaji. Kwa maana hiyo siyo mtu mzuri, hafai kwenye jamii.
Kwa mwenendo huo, naamini ndiyo maana ameporomoka, anakosa sifa ya kuitwa kioo cha jamii. Inawezekanaje awe mfano wa kuigwa ikiwa yeye ni kirusi katika hiyohiyo jamii? Mtu unajua kabisa hii mali ya wizi unainunua kwa bei chee halafu unaona raha.
Kununua mali ya wizi ni hujuma nzito, ni ukosefu wa huruma kwa sababu wakati wewe unauziwa mali hizo kwa bei nafuu sawa na bure, halafu unaitumia kwa nafasi huku ukijionesha, mwenzako anateseka mno.
Fikiria kama wewe umejibana, ukajitutumua kununua simu aina ya iPhone 5 kwa shilingi milioni 1.6. Umeitumia wiki mbili tu unaibiwa, halafu mtu mwingine anakuja kuuziwa kwa shilingi 400,000  au 300,000. Itakuuma kiasi gani?
Bila shaka utamchukia mwizi na yule aliyeuziwa, kwani angekuwa muungwana asingekubali kununua. Laiti angekuwa raia mwema, angesaidia huyo muuzaji akamatwe ili aliyeibiwa arudishiwe mali yake. Kutumia mali ya wizi ni dhuluma, ni wizi.
Uwoya alikamatwa na simu ya wizi aina ya iPhone 5, kwa hiyo kama aliuziwa, na kwa mujibu wa tafsiri ambayo nimeielezea hapo juu ni wazi kwamba yeye siyo raia mwema. Ukweli uzidi kusimama kwamba hafai kuitwa kioo cha jamii.
Je, ni tamaa ya kutaka vitu vizuri wakati pesa hana? Ajioneshe mjini kwamba anamiliki iPhone 5 kumbe ni ya wizi, ameipata kimagumashi. Namshauri Uwoya aache mtindo wa kuishi kimagumashi, kama hana akubali hali halisi. Si kulazimisha maisha ya gharama, matokeo yake ndiyo haya.

ANGEMTII MUMEWE YASINGEMFIKA HAYA
Nikiongoza jopo la waandishi kutoka Global Publishers Ltd, mwaka jana, tulifanikisha kumsuluhisha Uwoya na mumewe, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ kutokana na mgogoro wa nguvu ambao ulikuwa unaitikisa ndoa yao. 
Malalamiko ya Kataut yalijikita katika uaminifu, kwamba Uwoya alikuwa anaonesha alama nyingi kuwa si mwaminifu kwenye ndoa yao. Mume huyo, alisema kwamba amenunua vifaa na kuanzisha kampuni ili mkewe ajisimamie katika kazi zake za filamu lakini mke hataki.
“Analipwa pesa kidogo ambayo akifanya shopping tu zinakwisha, maprodyuza wanapata fedha nyingi, yeye anafanya kazi, anauza sura tu lakini pesa hakuna. Nataka atengeneze filamu zake ili apate pesa za kuonekana lakini haelewi wakati kila kitu nimeshanunua,” Kataut alilalamika.
Kataut alikuwa na nia ya dhati kabisa ya kumwokoa Uwoya na pengine kama angefuata mwongozo wa mumewe leo hii asingeporomoka kama alivyo. Pengine yanayomkuta leo ni malipo ya kile ambacho alimtendea mwanamme huyo.
Mke wa mtu kunaswa hotelini na kijana wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, ni aibu sana! Kabla ya hapo zilishaibuka stori kwamba amegombana na supastaa Jacqueline Wolper kisa mwanaume. Alimtesa sana Kataut wa watu.
Akiwa yupo ndani ya ndoa, akaingia kwenye mgogoro na boyfriend wake wa zamani, Hamis Ramadhan Baba ‘H-Baba’, akadai eti katika wanaume wake wote waliopita, ambaye hawezi kurudiana naye ni H-Baba. Huyu ni mke wa mtu.
Tafsiri; kumbe pamoja na kuwa kwenye ndoa, anaweza kurudiana na wanaume wake wote waliotangulia isipokuwa tu H-Baba. Je, unamuonaje huyo? Ni mke wa mtu kweli? 
Mke wa H-Baba, Flora Mvungi naye akamvaa Uwoya, akamchamba, wakachambana. Mke wa mtu anagombana na mwanamke mwingine kisa mwanaume tofauti na mumewe. Ninaposema hafai kwenye jamii namaanisha kweli.
Matukio ambayo anakumbana nayo hususan hili la wizi wa simu, achukue kama changamoto na ajisahihishe pale alipojikwaa. Amwangukie mumewe pengine mambo yakamnyookea. Iwe kama ameiba yeye moja kwa moja au aliuziwa, ajisahihishe. 

Source:Global Publishers

No comments:

Post a Comment