MKUU wa Kaya ya Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa mkoani
Mtwara, Bibi Somoe Mtiti (106) amenusurika ‘kutekwa’ na mtu anayeaminika
na wakazi wa eneo hilo kuwa ni mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa
baada ya wananchi kuvamia gari lake na kuliteketeza kwa moto jana usiku.
Hivi karibuni Bibi Mtiti aliionya Serikali
juu ya mpango wake wa kusafirisha gesi ghafi kwenda Dar es Salaam kwa
madai iwapo itapuuza onyo hilo bomba hilo litasafirisha maji badala ya
gesi iliyokusudiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria
Nzuki alisema hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kwa kuwa
mhusika hajakwenda polisi kulalamika.
Kwa mujibu wa wanakijiji hao, mtu huyo ambaye
ana asili ya kijiji hicho waliyemtambua (jina linahifadhiwa) aliwasili
kijijini hapo jana saa 10 jioni akiwa na gari dogo aina ya Mark II na
kwenda nyumbani kwa shangazi yake.
Habari zinadai kuwa saa 2 usiku mshukiwa huyo alidaiwa kwenda nyumbani kwa Bibi Mtiti akiwa na gari pamoja na shangazi yake. “Unajua
yule bibi tunamlinda, sasa ilipoonekana ile gari usiku pale, watu
wakaanza kujiuliza linafanya nini…wakaanza kusogea, kadiri muda
ulivyokuwa unakwenda ndivyo watu walivyozidi kuongezeka,”alisema Juma
Ayoub mkazi wa kijiji hicho.
Asha Hamisi ni mtoto wa pili wa Bibi Mtiti,
akihadithia juu ya tukio hilo, alisema yapata saa 2 usiku wakiwa
wanakula chakula walipokea wageni wawili ambao baada ya kumaliza kula
waliomba kuongea na mkuu huyo wa kaya.
“Alikuja kijana na mama wakaniomba kuongea na
bibi…alimuuliza bibi kama ana uwezo wa kwenda Mtwara, bibi akajibu
hawezi…wakaniuliza mimi kama naweza kwenda badala yake nikawaambia
siwezi…akasema ametumwa na Rais Jakaya Kikwete na Hawa Ghasia...wamjie
bibi wakazungumze naye mambo ya gesi,” alisema Hamis.
Aliongeza kuwa “Kama bibi yupo tayari Jumanne
ijayo watamfuata kwa gari…mimi nikasema sitaki…nilipochungulia nje
nikaona watu wengi wamezunguka.”
Kwa upande wa mtoto mwingine wa bibi huyo
alisema,” Kwa kuwa tunamfahamu tulimwambia aondoke mpango aliojia
haufai, akawa anabisha, tukaendelea kumsihi..wakati huo watu wanazidi
kuongezeka…alipotoka akakosea njia, alipopita hakukuwa na njia…watu
walimfuata wakaanza kumrushia mawe…aliacha gari akakimbia…ndipo wananchi
walipoliteketeza gari kwa moto,” alisema Manzi Mohamedi Faki mtoto wa
tano wa Bibi Mtiti.
Shangazi wa mtuhumiwa amethibitisha kumpokea
mwanaye huyo na kumsindikiza kwa Bibi Mtiti na ambako alimwomba mkuu
huyo wa kaya akubali kuondoka naye kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kuwa
ametumwa na viongozi wake wa juu.
“Ni mwanangu mtoto wa kaka yangu, alikuja
akaniomba nimepeleke kwa bibi akamsalimie tuliondoka saa 2 usiku…watu
walituzingira na hali ilipokuwa mbaya niliondoka na kumwacha mwanangu
pale, naye
alikimbia na ndipo walipochoma moto gari,” alisema shangazi
huyo. Alifafanua kuwa “Huyu mwanangu anaishi Dar es Salaam, anafanya kazi Usalama wa Taifa…nadhani alirudi jana hiyohiyo Mtwara.'' |
No comments:
Post a Comment