MAUAJI YA KUTISHA YATOKEA WILAYANI RUNGWE MKOANI MBEYA.TUNAOMBA RADHI KWA PICHA HIZI !!
MATUKIO ya kutisha na ya kinyama
dhidi ya watoto wadogo yameendelea kuutikisa Mkoa wa Mbeya, baada ya mwanafunzi
wa chekechea, Ayoub Agen (6) kuuwa kwa kuchinjwa mithili ya kuku na wauaji
kuondoka na kichwa chake.
Hata hivyo wananchi wenye hasira
walifanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo, ambaye hata hivyo jina
lake halikuweza kupatikana ambapo baada ya kummbana ili aeleze sehemu
walikokificha kichwa cha marehemu aligoma hivyo kuamua kumteketeza kwa
moto.
Habari za uhakika kutoka eneo la
tukio na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji cha Ijoka katika kata ya
Mpombo, wilayani Rungwe, Rafael Mwaikenda, zinadai kuwa tukio hilo
lilitokea Machi 31 majira ya saa 11:00 jioni.
Akifafanua zaidi Mwenyekiti
huyo alisema, marehemu Agen alikuwa ni mwanafunzi wa chekechea
katika shule ya msingi Lusanje kijijini hapo na kwamba alikutwa na mauti hayo
ya kikatili baada ya watu hao wasiofahamika kufanikiwa kumuiba nyumbani kwao.
Mwaikenda alisema mwili wa
marehemu uliokotwa ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili huku kichwa kikiwa
hakionekani hadi sasa ikiwa ni muda mfupi tu baada ya watu hao wasiofahamika
kumwiba toka nyumbani kwa wazazi wa marehemu .
“Marehemu alichukuliwa na watu hao
wasiofahamika akiwa anacheza na wenzake na wenzake baada ya kuona hivyo
waliamua kutoa taarifa ambapo muda mfupi walianza kumtafuta bila mafanikio,
lakini wananchi wakiwa wanaendelea na harakati hizo waliukuta mwili huo ukiwa
umetelekezwa kichakana na wauaji hao kuondoka na kichwa” alifafanua Mwaikenda.
Mkazi mwingine katika kijiji hicho,
Tumpale Sankemwa, alikielezea mkasa huo, alisema baada ya wananchi kugundua
mwili huo wa marehemu waliendelea kuwasaka wahusika na wakiwa katika harakati
hizo ghafla walikutana na mtu mmoja ambaye walimtilia mashaka.
Alisema baada ya kumfanyia
mahojiano ya kina kwa kuwa alikuwa hafahamiki na mgeni kijijini hapo, alikuwa
akijibu jeuri hivyo kuwapandisha hasira wananchi jambo lililosababisha kuanza
kumshambulia na hatimaye kumuua papo hapo.
Hata hivyo alisema wakati wananchi
wakiendelea kumshushia kipigon mtu huyo licha ya kutotaja jina lake, alikiri
kuhusika katika tukio hilo kwa kueleza kuwa waliohusika walikuwa watatu na
kwamba wenzake walikuwa wameondoka.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,
Kamishina Msaidizi wa jeshi la polisi,Diwani Athumani, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba hadi sasa kichwa cha marehemu huyo hakijaonekana na
jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi.
“Ni kweli tukio hilo limetokea,
hata hivyo mtu anayetuhumiwa kushiriki mauaji hayo naye aliuawa kwa kupigwa na
wananchi wenye hasira ambao licha ya kumuua waliuteketeza mwili wake kwa
moto”.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa wa mauaji
hayo ni mwanaume anayekadiliwa kuwa na miaka kati ya 30 hadi 35 na kwamba
uchunguzi wa awali umeonesha chanzo cha mauaji hayo kinahusishwa na imani
za kishirikina.
No comments:
Post a Comment