Wachezaji watano wa timu ya Young
Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea
kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka
2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji ambao mpaka sasa
wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young Africans ni walinzi
Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo
Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na
Jerson Tegete (2014-2016).
Mwenyekiti
wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb
amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote
na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka
2016.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine,
mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua
tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda
mrefu "alisema Bin Kleb.
Wakati huo huo kikosi cha Young Africans
leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini
Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14,
2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya
kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Aidha Uongozi wa klabu
ya Young Africans unampa pongezi beki wake wa kati Kelvin Patrick
Yondani mchezaji bora wa mwaka 2012/2013 kwa kuteuliwa kuwa nahodha mpya
wa timu ya Taifa Tanzania bara (Kilimanjaro stars) inayokwenda
kushiriki mashindano ya Chalenji jijini Nairobi.
Kelvin Yondani
ametambulishwa rasmi leo na kocha mkuu wa timu ya Taifa Kim Poulsen kwa
waandishi wa habari katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa timu ya Taifa
wanaokwenda nchini Kenya katika hoteli ya Accomondia eneo la gerezani
jijini Dar es salaam.
Tunapenda
kumpa pongezi kijana wetu, mchezaji wetu Yondani kwa kupewa nafasi hiyo
kubwa katika timu ya Taifa, tunamtakia kila la kheri na awe kiongozi
bora kwa wachezaji wenzake na kuiwakilisha vizuri nchi yetu na timu yake
ya Young Africans.
No comments:
Post a Comment